Nehemiah 9:25-35

25 aWakateka miji yenye ngome na nchi yenye rutuba, wakamiliki nyumba zilizojazwa na vitu vizuri vya kila aina, visima vilivyochimbwa tayari, mashamba ya mizabibu, mashamba ya mizeituni na miti yenye matunda kwa wingi. Wakala, wakashiba nao wakanawiri sana, wakajifurahisha katika wema wako mwingi.

26 b“Lakini hawakukutii nao wakaasi dhidi yako, wakatupa sheria zako nyuma yao. Wakawaua manabii wako, waliowaonya ili wakurudie, na wakafanya makufuru makubwa. 27 cHivyo ukawatia mikononi mwa adui zao, ambao waliwatesa. Lakini walipoteswa, wakakulilia wewe. Kutoka mbinguni uliwasikia, nawe kwa huruma zako kuu ukawapa waokozi, waliowaokoa kutoka mikononi mwa adui zao.

28 d“Lakini mara walipokuwa na raha, wakafanya maovu tena machoni pako. Kisha ukawaacha mikononi mwa adui zao, nao wakawatawala. Walipokulilia tena, ukasikia kutoka mbinguni, na kwa huruma zako ukawaokoa kila mara.

29 e“Ukawaonya warudi katika sheria yako, lakini wakawa na kiburi na hawakutii amri zako. Wakatenda dhambi dhidi ya maagizo yako ambayo kwayo mtu ataishi kama akiyatii. Kwa ukaidi wakakugeuzia kisogo, wakawa na shingo ngumu na wakakataa kusikiliza. 30 fKwa miaka mingi ulikuwa mvumilivu kwao. Kwa njia ya Roho wako ukawaonya kupitia manabii wako. Hata hivyo hawakujali, basi ukawatia mikononi mwa mataifa jirani. 31 gLakini kwa rehema zako kuu hukuwakomesha wala kuwaacha, kwa kuwa wewe ni Mungu mwenye neema na rehema.

32 h“Basi sasa, Ee Mungu wetu, uliye mkuu, mwenye nguvu na Mungu wa kuogofya, mwenye kushika agano lake la upendo, usiache taabu hizi zote zionekane kuwa kitu kidogo mbele za macho yako, taabu hizi zilizotupata, juu ya wafalme wetu na viongozi, juu ya makuhani wetu na manabii, juu ya baba zetu na watu wako wote, tangu siku za wafalme wa Ashuru hadi leo. 33 iKatika hayo yote yaliyotupata, umekuwa mwenye haki, na umetenda kwa uaminifu, wakati sisi tumetenda mabaya. 34 jWafalme wetu, viongozi wetu, makuhani wetu na baba zetu hawakufuata sheria yako. Hawakuzingatia amri zako wala maonyo uliyowapa. 35 kHata walipokuwa wangali katika ufalme wao, wakiufurahia wema wako mkuu katika nchi kubwa na yenye rutuba uliyowapa, hawakukutumikia wala kugeuka kutoka njia zao mbaya.

Copyright information for SwhNEN